AI-assisted research summary: Rais ametangaza tarehe 27 Novemba 2024 kuwa siku ya mapumziko.
ISSN 0856 - 034X THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA Supplement No. 43 22nd November, 2024 SUBSIDIARY LEGISLATION To The Gazette of the United Republic of Tanzania No. 47 Vol. 105 Dated 22nd November, 2024 Printed by The Government Printer, Dodoma by Order of Government TANGAZO LA SERIKALI NA. 956 la tarehe 22/11/2024 SHERIA YA SIKUKUU ZA KITAIFA, (SURA YA 35) _______ TAMKO _______ (Limetolewa chini ya kifungu cha 3) TAMKO LA KUTANGAZA SIKU YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA KUWA SIKU YA MAPUMZIKO LA MWAKA 2024 KWA KUWA kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa, Sura ya 35, kinampa Rais mamlaka ya kutangaza siku yoyote kuwa siku ya mapumziko kama nyongeza ya siku zilizoainishwa kwenye Jedwali la Sheria hiyo au kubadili siku yoyote kati ya zilizoainishwa na siku nyingine na siku hiyo kuwa siku ya mapumziko kama vile imetajwa kwenye Jedwali la Sheria; NA KWA KUWA tarehe 27 Novemba, 2024, Jumatano, ambayo ni siku ya kazi, imetangazwa na Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa kuwa Siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024; NA KWA KUWA kwa madhumuni ya kuwezesha watu wote wenye sifa ya kupiga kura kutumia haki yao ya kupiga kura na KWA KUWA kuifanya siku hiyo ya uchaguzi kuwa siku ya mapumziko kutatoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika kupiga kura, Rais anakusudia kutangaza Siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwa siku ya mapumziko; KWA HIYO BASI, kwa mamlaka aliyopewa Rais chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa, Sura ya 35, mimi, SAMIA SULUHU HASSAN, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa Tamko kuwa tarehe 27 Novemba, 2024 itakuwa siku ya mapumziko. Tamko hili limetolewa na kuwekewa Lakiri ya Umma leo tarehe 22 Novemba 2024. DODOMA SAMIA SULUHU HASSAN, Rais